‘Baki kwenye sera': Wapiga kura hawataki vioja katika mdahalo wa Harris-Trump

DCX
  • Author, Rachel Looker
  • Nafasi, BBC

Mara ya mwisho wagombea wa urais wa Marekani walipokutana jukwaani, walibezana na kushambuliana katika mdahalo. Kubabaika kwa Rais Joe Biden kulimlazimisha kujiondoa kwenye kinyang'anyiro hicho.

Kwa hivyo sasa Kamala Harris, mbadala wake kama mteule wa Democratic, atapambana dhidi ya Rais wa zamani Donald Trump katika mdahalo wa pili tarehe 10 Septemba.

BBC ilizungumza na wapiga kura kutoka katika nyanja mbalimbali za kisiasa. Haya ndiyo mambo wanayotarajia kuyaona katika mdahalo.

Pia unaweza kusoma

Robert Oliver 27

Mfuasi wa Republican huko Utah, alimpigia kura Biden katika uchaguzi wa 2020 lakini anapanga kumpigia Trump mwezi Novemba.

Nina hamu ya kuona kile ambacho wote wawili watafanya. Kamala Harris amepigiwa upatu hivi karibuni dhidi ya Donald Trump, ambaye mara nyingi huangushwa kwa sababu ya mtindo wake wa kufanya mijadala na sauti yake.

Nimeamua kumpigia kura Trump mara hii, lakini nataka kuona kile ambacho makamu wa rais atakisema. Nitapenda kuona anavyozungumza bila ya kusoma sehemu. Ninataka kuona anavyojibu maswali mbele ya Trump.

Ingawa ninampigia kura Trump, lakini sio kwa sababu najiamini naye. Natumai Trump asimame pale na asiwe mwendawazimu kwa chochote kile na apunguze mashambulizi na kuzingatia sera.

Daniel Crumrine 28

Mkaazi wa Colorado, alimpigia kura Biden katika uchaguzi uliopita wa urais. Ana hamu ya kutazama mjadala.

Ninahisi kama najua kitakachotokea. Ninajua kuwa Kamala Harris ni mzungumzaji mzuri kwenye mdahalo. Bado ninakumbuka mjadala wake na Mike Pence wa miaka minne iliyopita na ninafurahi sana kumuona akijadiliana na Trump. Nina furaha kuwa na mtu kwenye jukwaa ambaye ataweza kushindana na Trump moja kwa moja jukwaani.

Mtego mkubwa ni kwamba Donald Trump anasema mambo mengi kwa wakati mmoja. Ni rahisi kuingia kwenye mtego katika kile anachosema. Natumai Harris hatazama kwenye mtego wake. Ningependa kumuona akiendelea kutoa ujumbe wake wa matumaini na wa kusisimua hata mbele ya Trump.

Jessi Mazzoni 31

Mpiga kura huru kutoka jimbo la Pennsylvania, alimuunga mkono Biden mara ya mwisho lakini anapanga kumpigia kura mgombea wa tatu au kuandika jina la mgombea asiyekuwepo mwezi Novemba.

Kwa kweli sijapanga kutazama mjadala huo mubashara. Sifurahishwi na mgombea yeyote kati ya hao.

Kwa kile nilichoona kwenye mijadala yetu katika chaguzi chache zilizopita, ni majukwaa tu ya nani anayeweza kupiga kelele zaidi na nani aliye na maneno mazuri ambayo yataandikwa kwenye kichwa cha habari. Sijasikia chochote cha maana.

Ikiwa mtu atapanda jukwaani na akawa mkweli juu ya kile anachoweza kukifanikisha na kile asichoweza kukifanikisha, basi hilo lingebadilisha mawazo yangu. Lakini sidhani yoyote kati yao atasema kitu kama hicho.

Misty Dennis 45

Mpiga kura huyu wa chama cha Republican alimuunga mkono Trump mwaka wa 2016 na 2020. Anapanga kumpigia kura tena, lakini anataka kusikia zaidi kuhusu sera kutoka kwa wote wawili.

Ninaitazama kana ni mahojiano ya kazi, ni nani ninayemchagua kuwa rais. Kila siku, huzungumza na watu katika kiwango cha umaskini na hali inaonekana kuzidi kuwa mbaya. Binafsi nadhani uchumi ulikuwa bora chini ya Trump. Nataka kusikia Kamala Harris atafanya nini.

Nimekuwa nikisikia zaidi tu anavyo vuma na na huwezi kuiendesha Marekani kwa kuvuma pekee. Natarajia mjadala mzuri ambapo pande zote mbili zitaweka sera zao mezani.

Cannor Logan 23

Mwana Republican huyu alimpigia kura Trump 2020 - na anaamini uchumi ulikuwa bora zaidi chini ya utawala wa rais huyo wa zamani. Nadhani itakuwa mdahalo wa kuelimisha na kuburudisha.

Ningependa kujua jinsi uchumi wetu utakavyorudi kwenye mstari. Ningependa pia kujua kuhusu mipango ya wagombea ya kupunguza wahamiaji haramu.

Sera za Trump ziko wazi. Lakini nadhani Kamala Harris ameficha maoni yake au kubadili maoni. Trump anafanya kazi nzuri kuweka mipango yake. Lakini nadhani udhaifu wake mkubwa ni tabia yake.

Ninapanga kumpigia kura Trump tena na ninatumai atashinda mjadala, lakini hakuna mengi kati yao watafanya au kusema ili kubadilisha mawazo ya watu.

Felicity Felgate 33

Mpiga kura huru alimpigia kura Trump 2020 lakini kwa sasa hajaamua wa kumpigia.

Nina furaha zaidi kuwa tutakuwa na Kamala na nina furaha kwamba wafanya mdahalo vipaza sauti vikiwa vimezimwa ili wasiingiliane.

Wagombea hushambuliana sana. Hata katika mdahalo uliopita. Nilijiuliza: 'Hata wamejibu maswali? Wanashambuliana wenyewe kwa wenyewe badala ya kujibu yale ambayo tunayotaka kuyasikia.

Douglas Stewart 26

Mwanachama wa Democratic, alifurahi kuona Biden akiachia ngazi kama mteule na anaamini chama chake sasa kina nafasi nzuri zaidi ya kumshinda Trump.

Nina mpango wa kutazama mdahalo. Nadhani utendaji wa Biden ulikuwa wa kukatisha tamaa na kwa hivyo ninafurahi kuona kile ambacho Harris anaweza kukifanya, tabia na uwasilishaji wake.

Suala kubwa kwangu ni mabadiliko ya tabia nchi na sera ya mazingira, kwa hivyo natamani kusikia anasema nini juu ya hilo.

Hata hivyo, jambo la kusikitisha kwangu, ni kwamba nitampigia kura mtu yeyote atakayeshindana na Trump.

Pia unaweza kusoma

Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Seif Abdalla