Msalaba Quotes

Quotes tagged as "msalaba" Showing 1-5 of 5
Enock Maregesi
“Jina langu ni Enock Maregesi na ningependa kukwambia kisa kidogo kuhusiana na bibi yangu, Martha Maregesi. Mwanamke huyu alikuwa mke mwenye upendo usiokuwa na masharti yoyote. Alikuwa mama na bibi aliyefundisha familia yake umuhimu wa kujitolea na umuhimu wa uvumilivu. Ijapokuwa hakupendelea sana kujizungumzia mwenyewe, ningependa kukusimulia kisa kidogo kuhusiana na hadithi ya maisha ya mwanamke huyu wa ajabu katika maisha yangu.

Bibi yangu alizaliwa katika Kitongoji cha Butimba, Kijiji cha Kome, Kata ya Bwasi, Tarafa ya Nyanja (Majita), Wilaya ya Musoma Vijijini, Mkoa wa Mara, katika familia ya watoto kumi, mwaka 1930. Alisoma katika Shule ya Msingi ya Kome ambako alipata elimu ya awali na msingi na pia elimu ya kiroho kwani shule yao ilikuwa ya madhehebu ya Kisabato. Aliolewa na Bwana Maregesi Musyangi Sabi mwaka 1946, na kufanikiwa kupata watoto watatu; wa kiume wakiwa wawili na wa kike mmoja. Matatizo hasa ya bibi yalianza mwaka 2005, alipougua kiharusi akiwa nyumbani kwake huko Musoma. Hata hivyo alitibiwa hapo Musoma na Dar es Salaam akapona na kuwa mwenye afya ya kawaida. Lakini tarehe 19/10/2014 alipatwa tena na kiharusi na kulazwa tena katika Hospitali ya Mkoa ya Musoma, ila akajisikia nafuu na kuruhusiwa kurudi nyumbani – lakini kwa maagizo ya daktari ya kuendelea na dawa akiwa nje ya hospitali. Tarehe 29/10/2014 alirudi tena Hospitali ya Mkoa ya Musoma kwa tiba zaidi, lakini tarehe 4/11/2014 saa 7:55 usiku akafariki dunia; akiwa amezungukwa na familia yake.

Dunia ina watu wachache sana wenye matumaini na misimamo ya kutegemea mazuri, na wachache zaidi ambao wako tayari kugawa matumaini na misimamo hiyo kwa watu wengine. Nitajisikia furaha siku zote kwamba miongoni mwa watu hao wachache, hata bibi yangu alikuwemo. Msalaba uliwekwa wakfu na Mwenyezi Mungu baada ya mwili wa Yesu Kristo kuning’inizwa juu yake. Kwa kuwa bibi yangu ametanguliwa na msalaba, msalaba utamwongoza mahali pa kwenda.”
Enock Maregesi

Enock Maregesi
“Biblia pamoja na historia vinatwambia kuwa mitume kumi na wawili wa Yesu Kristo waliamua kufa kinyama kama mfalme wao alivyokufa, kwa sababu walikataa kukana imani yao juu ya Yesu Kristo.

Mathayo alikufa kwa ajili ya Ukristo nchini Ethiopia kwa jeraha lililotokana na kisu kikali, Marko akavutwa na farasi katika mitaa ya Alexandria nchini Misri mpaka akafa, kwa sababu alikataa kukana jina la Yesu Kristo.

Luka alinyongwa nchini Ugiriki kwa sababu ya kuhubiri Injili ya Yesu Kristo katika nchi ambapo watu hawakumtambua Yesu.

Yohana alichemshwa katika pipa la mafuta ya moto katika kipindi cha mateso makubwa ya Wakristo nchini Roma, lakini kimiujiza akaponea chupuchupu, kabla ya kufungwa katika gereza la kisiwa cha Patmo (Ugiriki) ambapo ndipo alipoandika kitabu cha Ufunuo. Mtume Yohana baadaye aliachiwa huru na kurudi Uturuki, ambapo alimtumikia Bwana kama Askofu wa Edessa. Alikufa kwa uzee, akiwa mtume pekee aliyekufa kwa amani.

Petro alisulubiwa kichwa chini miguu juu katika msalaba wa umbo la X kulingana na desturi za kikanisa za kipindi hicho, kwa sababu aliwaambia maadui zake ya kuwa alijisikia vibaya kufa kama alivyokufa mfalme wake Yesu Kristo.

Yakobo ndugu yake na Yesu (Yakobo Mkubwa), kiongozi wa kanisa mjini Yerusalemu, alirushwa kutoka juu ya mnara wa kusini-mashariki wa hekalu aliloliongoza la Hekalu Takatifu (zaidi ya futi mia moja kwenda chini) na baadaye kupigwa kwa virungu mpaka akafa, alipokataa kukana imani yake juu ya Yesu Kristo.

Yakobo mwana wa Zebedayo (Yakobo Mdogo) alikuwa mvuvi kabla Yesu Kristo hajamwita kuwa mchungaji wa Injili yake. Kama kiongozi wa kanisa hatimaye, Yakobo aliuwawa kwa kukatwa kichwa mjini Yerusalemu. Afisa wa Kirumi aliyemlinda Yakobo alishangaa sana jinsi Yakobo alivyolinda imani yake siku kesi yake iliposomwa. Baadaye afisa huyo alimsogelea Yakobo katika eneo la mauti. Nafsi yake ilipomsuta, alijitoa hatiani mbele ya hakimu kwa kumkubali Yesu Kristo kama kiongozi wa maisha yake; halafu akapiga magoti pembeni kwa Yakobo, ili na yeye akatwe kichwa kama mfuasi wa Yesu Kristo.

Bartholomayo, ambaye pia alijulikana kama Nathanali, alikuwa mmisionari huko Asia. Alimshuhudia Yesu mfalme wa wafalme katika Uturuki ya leo.
Bartholomayo aliteswa kwa sababu ya mahubiri yake huko Armenia, ambako inasemekana aliuwawa kwa kuchapwa bakora mbele ya halaiki ya watu iliyomdhihaki.

Andrea alisulubiwa katika msalaba wa X huko Patras nchini Ugiriki. Baada ya kuchapwa bakora kinyama na walinzi saba, alifungwa mwili mzima kwenye msalaba ili ateseke zaidi. Wafuasi wake waliokuwepo katika eneo la tukio waliripoti ya kuwa, alipokuwa akipelekwa msalabani, Andrea aliusalimia msalaba huo kwa maneno yafuatayo: "Nimekuwa nikitamani sana na nimekuwa nikiitegemea sana saa hii ya furaha. Msalaba uliwekwa wakfu na Mwenyezi Mungu baada ya mwili wa Yesu Kristo kuning’inizwa juu yake." Aliendelea kuwahubiria maadui zake kwa siku mbili zaidi, akiwa msalabani, mpaka akaishiwa na nguvu na kuaga dunia.

Tomaso alichomwa mkuki nchini India katika mojawapo ya safari zake za kimisionari akiwa na lengo la kuanzisha kanisa la Yesu Kristo katika bara la India.

Mathiya alichaguliwa na mitume kuchukua nafasi ya Yuda Iskarioti, baada ya kifo cha Yuda katika dimbwi la damu nchini India. Taarifa kuhusiana na maisha na kifo cha Mathiya zinachanganya na hazijulikani sawasawa. Lakini ipo imani kwamba Mathiya alipigwa mawe na Wayahudi huko Yerusalemu, kisha akauwawa kwa kukatwa kichwa.

Yuda Tadei, ndugu yake na Yesu, aliuwawa kwa mishale alipokataa kukana imani yake juu ya Yesu Kristo.

Mitume walikuwa na imani kubwa kwa sababu walishuhudia ufufuo wa Yesu Kristo, na miujiza mingine. Biblia ni kiwanda cha imani. Tunapaswa kuiamini Biblia kama mitume walivyomwamini Yesu Kristo, kwa sababu Biblia iliandikwa na mitume.”
Enock Maregesi

Enock Maregesi
“Yesu wakati anakufa msalabani hakufikiria kifo. Alifikiria maisha.”
Enock Maregesi

Enock Maregesi
“Kuna ushahidi wa kutosha katika maandiko kwamba Yesu aliugua hipovolimia kutokana na kuchapwa. Yesu alipobeba msalaba wake kuelekea Golgotha alianguka, na mtu mmoja aliyeitwa Simoni alilazimishwa ama kuubeba au kumsaidia Yesu kuubeba msalaba huo hadi kilimani. Kuanguka huko kunaonyesha kwamba Yesu alikuwa na shinikizo la damu. Alama nyingine inayoonyesha kwamba Yesu alipatwa na ugonjwa wa hipovolimia ni pale alipodai kuwa alikuwa na kiu, akiwa msalabani, akimaanisha kiu ya maji.”
Enock Maregesi

Enock Maregesi
“Adui wa msalaba ni yule anayeipenda dunia badala ya Mungu, na rafiki wa msalaba ni yule anayempenda Mungu badala ya dunia.”
Enock Maregesi